Thursday, March 30, 2023

SERIKALI YABORESHA MAZINGIRA YA WAFANYABIASHARA WADOGO (MACHINGA)

"Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wadogo (Machinga, Mama lishe, Baba lishe na Waendesha bodaboda, bajaji na maguta)".
Dkt. Samia Suluhu Hassan 
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametanabaisha kuwa wamachinga ni watu muhimu katika kukuza pato la Taifa na takwimu zinaonesha kuwa sekta ya viwanda vidogo na biashara ndogo imetengeneza ajira, kukuza uchumi na kuondoa umasikini. Aidha, amesisitiza kwamba wamachinga ni watu muhimu sana na wamekuwa suluhisho la mahitaji kwa watu wengi kuanzia wenye kipato cha chini, kati na kipato cha juu, hivyo ametoa rai kwa Watanzania wote kuendelea kuunga mkono shughuli zao kwa vitendo. 

Serikali imeziagiza mamlaka zinazohusika na ujenzi wa masoko mazuri unaoendelea kwenye maeneo mbalimbali nchini wazingatie na waandae miundombinu kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga.

Sekta hiyo ina jumla ya wajasiriamali milioni 3.1 ambao wameajiriwa ni asilimia 23.4 ya nguvu kazi ya Taifa na imechangia asilimia 27 katika pato la Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan ameahidi kutoa shilingi milioni 10 kwa ajili kutatua
changamoto ya uendeshaji wa ofisi za Machinga mikoani.
Ahadi hiyo aliitoa alipozungumza kwa njia ya simu na Viongozi wa
Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Mei 06, 2022 kupitia kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati wa mkutano wa mafunzo kwa viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (Shiuma) kutoka mikoa yote Tanzania uliofanyika Jijini Dodoma.

Rais Dkt. Samia alibainisha kuwa, fedha hizo zitaanza kutolewa katika mwaka wa
fedha ulioanza mwezi Julai, 2022.

Sambamba na hilo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa nchini kuwapanga wamachinga katika maeneo stahiki bila kusababisha vurugu.
Dkt. Samia amesema licha ya serikali kutoa fursa kufanya biashara kama njia ya ajira kwao, ni lazima Serikali iwatengenezee mazingira rafiki nasio kufanya biashara kiholela kwenye maeneo yasiyo na usalama na utulivu kwao na mali zao.
Mfano wa masoko maalumu ya wamachinga yaliyojengwa kufuatia agizo la Rais Dkt. Samia ni Ujenzi wa
soko la wazi la Machinga lau Jijijni Dodoma ambao umegharimu kiasi cha
shilingi bilioni 9.53 mpaka kukamilika kwake ambapo
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa shilingi bilioni tatu
na Halmashauri ya Jiji ilitoa kiasi cha shilingi bilioni
sita na nusu kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri.
Aidha, Rais Dkt. Samia wakati akizungumza na jamii ya wafanyabiashara ndogondogo (Wamachinga) alipowaalika Ikulu ya Dar Es Salaam, Rais Dkt. Samia alisema Serikali
yake imeshaanza kulifanyia kazi suala la kuyaboresha mazingira wafanyiayo kazi machinga kwa kutenga fedha
kwa ajili ya kuboresha baadhi ya masoko, ikiwemo
la Karikakoo.
Alitanabaisha kuwa ujenzi wake ukikamilika litakuwa na
uwezo wa kuchukua wafanyabiashara zaidi ya 4,000
ikilinganishwa na idadi ya 2,500 iliyokuwepo awali.
Rais Dkt. Samia amesema, Serikali inaendelea kutafuta
maeneo ya wazi, kwa ajili ya kujenga masoko katika
maeneo ya pembezoni mwa Miji, ili kuondoa
msongamano wa wateja katika masoko
yaliyokuwepo katikati ya Miji.

WALIOFELI, WALIOPATA MIMBA RUKSA KURUDI SHULE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeamua kuwapa nafasi ya pili wanafunzi wote wa shule za msingi nchini ambao walipata changaoto mbalimbali zilizowakwamisha kuendelea na masomo yao ikiwemo mimba, utoro na kufeli mtihani wa darasa la saba kurudi shule kwaajili ya kusoma na kufanya tena mtihani huo.
Rais Samia alisema kwamba uzoefu unaonyesha kwamba kundi la watoto wa kike wanaoshindwa shule ya msingi sababu ya kupata ujauzito huwa hawaendelei na masomo hata baada ya kujifungua tofauti na wale wa sekondari ambao wengi wao hurudi na kuendelea na masomo yao mpaka ngazi za juu za elimu.

 Rais Samia alisema kwamba Serikali imeamua kutoa fursa ya kuwarudisha shule wanafunzi wote walioacha na kufeli ili kuhakikisha watoto wa kitanzania wanajikwamua kielimu.
“Tumeamua watoto wote ambao waliacha shule kwa sababu mbalimbali na wale waliodondoka kwenye mtihani wa darasa la saba tuwape nafasi nyingine ya kurudi shule na kufanya tena mtihani huo, kwa wale ambao wanaona hawawezi kurudi tena shule tumewawekea mpango mwingine unaitwa elimu mbadala ‘altenative education’ watakwenda kwenye mkondo huo ili wakitoka hapo waweze kufanya miradi itakayowasaidia kujitunza”,alisema Rais Samia.
Aidha, aliongeza kuwa suala la kuwarudisha shule watoto wa kike walioacha sababu ya kupata ujauzito lisiwaletee mashaka  na kuwapotezea  muda Watanzania kwa kuanza kulijadili kwani Serikali imejipanga na imeona mifano kutoka kwenye nchi nyingine zinazofanya hivyo na kupata uhakika halitaleta uhalibifu wowote ndani ya mfumo wa elimu kutoka shule za msingi mpaka sekondari.
Rais Dkt. Samia aliiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi yenye dhamana kuandaa historia ya shule hiyo na kuiweka kwenye maktaba shuleni hapo ili watoto  watakaosoma shule hiyo waijue na kuienzi  pamoja na kuweka kumbukumbu za uhusiano mzuri na wa kindugu uliopo kati ya Tanzania na Uganda.

Wednesday, March 29, 2023

CHIFU HANGAYA "Nyota ya asubuhi inayong'aa"

SAMIA AWAASA MACHIFU, VIONGOZI WA DINI KUTETEA MILA NA UTAMADUNI WA MTANZANIA 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema pamoja na kuwa Utamaduni hutangaza mila na desturi za nchi lakini pia ni biashara na chanzo kikubwa cha mapato kwa sababu ni moja ya vivutio vya utalii.
Mhe. Rais Samia aliyasema hayo Septemba 08, 2021 katika Viwanja vya Red Cross Kisesa, Magu Jijini Mwanza wakati akifungua Tamasha la Utamaduni lilioandaliwa na Umoja wa Machifu Tanzania.

Katika Tamasha hilo, Machifu walimtawaza Mhe. Rais Dkt. Samia kukwa Chifu Mkuu wa Machifu wote nchini na kumpa jina la Chifu Hangaya likiwa na maana ya Nyota ya asubuhi inayong’aa.
Mara baada ya kutawazwa kuwa Chifu Mkuu Hangaya, Mhe. Rais Samia amewashukuru Machifu hao kwa heshima waliyompa na kuwaahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuwaletea maendeleo Watanzania. 
Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia amesema Serikali imejipanga kupanua wigo wa vivutio vya utalii, ukiwemo utalii wa utamaduni ambapo tayari ameanza kuchukua hatua za kutangaza vivutio vya utalii, biashara na uwekezaji kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour.
 Mhe. Rais Samia amewaomba Machifu hao nchini kwa kushirikiana na Serikali kudumisha amani na usalama ikiwa ni pamoja na kusuluhisha migogoro kwenye jamii zinazowazunguka.
Hamasa ya Rais Dkt. Samia kuhusu kuzingatia mila, desturi, utamaduni na maadili ya Kitanzania huitoa mara kwa mara kwani ni jambo lenye tija kwa Taifa. Itakumbukwa Novemba 19, 2022 katika hafla ya Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Kazi ya Utume na Huduma ya Kanisa la Waadventista wa Sabato yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, Jijini Dodoma, Raia Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa wito kwa viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali kuwahimiza waumini wa dini zao kuzingatia mila, utamaduni na maadili ya Kitanzania.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewataka Viongozi wa dini kuendelea kuwaandaa watoto na vijana katika malezi yenye maadili na tabia njema ambayo yatawajenga kuwa wazalendo kwa nchi yao.

Friday, March 10, 2023

4R: FALSAFA 4 ZA SAMIA | BINGWA WA DEMOKRASIA NA UTAWALA BORA

Falsafa ya 4R iliyoasisiwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan yenye maneno manne ya msingi ya kuzingatiwa ambayo ni;  Maridhiano (Reconciliation), Ustahimilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms) na Ujenzi mpya (Rebulding) 
ndio falsafa mashuhuri nchini Tanzania ambayo ndio hasa kitambulisho kinachomtambulisha Rais Dkt Samia ni gwiji wa siasa za maridhiano. 
Falsafa hii ameijenga tangu siku ya kwanza anaapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 19, 2021 alipotoa hotuba yake ya kwanza na kuliambia Taifa maneno yenye suluhu ndani yake, namnukuu.. ""Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama Taifa, ni wakati wa kufarijiana, kuoneshana upendo, udugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na Utanzania wetu. Huu sio wakati wa kutazama mbele kwa mashaka, bali ni wakati wa kutazama mbele kwa matumaini na kwa kujiamini. Sio wakati wa kutazama yaliyopita bali ni wakati wa kutazama yajayo" mwisho wa kunukuu. 
Aidha, tukiitazama Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Aprili 22, 2021 wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitanabaisha maono yake kuhusu hali ya demokrasia nchini kwa kuyasema yafuatayo, namnukuu.. "Maeneo mengine ni pamoja na kuendelea kulinda misingi 
ya demokrasia na uhuru wa watu pamoja na vyombo vya 
habari. Kama mnavyofahamu, uhuru na demokrasia ni msingi 
wa amani katika nchi na pia vinasaidia kuchochea maendeleo ya 
kisiasa, kiuchumi na kijamii. Hata hivyo, naomba niseme kuwa, 
hakuna uhuru ama demokrasia isiyolindwa na kusimamiwa na 
Sheria, Taratibu na Kanuni. Hivyo basi, pamoja na demokrasia 
na uhuru wa watu, niwaombe Watanzania tujidhatiti kufanya 
shughuli zetu tukizingatia masharti ya sheria za nchi. Hapa 
nakusudia kukutana na Viongozi wa vyama vya Siasa Tanzania 
ili kwa pamoja tuweke mwelekeo wa kuendesha shughuli za 
kisiasa zenye tija na maslahi kwa nchi yetu" mwisho wa kunukuu.
 
Hotuba hizi zinadhihirisha Rais Dkt. Samia kwenye upande wa Demokrasia na Utawala bora ni kinara.
Falsafa ya 4R (Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding) kwa upana na ufafanuzi wake Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameielezea kama ifuatavyo; Kuhusu Maridhiano (Reconciliation) alitaka kuhimizwa umoja na amani katika Taifa kwa kuhuisha moyo wa kitaifa na kuinganisha nguvu ya pamoja katika kuleta maendeleo.
Alisisitiza umuhimu wa kuachana na migogoro na mifarakano na kutembea pamoja na kufika pamoja katika safari ya kuleta maendeleo endelevu ya Taifa letu. 
Akizungumzia Ustahimilivu (Resilience) amesisitiza umuhimu wa kuzitumia changamoto kama fursa katika kuleta maendeleo kwani katika dunia ya sasa changamoto haziepukiki kwani ni dunia ya sayansi na teknolojia na lazima tukabiliane na kila changamoto kwa Ustahimilivu.

Kuhusu Mabadiliko (Reforms) aliwataka Watanzania kutokuwa watumwa wa historia na lazima kuwa tayari kwa mabadiliko pale yanapohitajika ili kuyafanya mambo kwenda mbele. 
Pia aliwataka Watanzania kuwa tayari kujifunza kutoka nchi na jamii nyingine zilizofanikiwa kama China, Singapore na Thailand.

Akizungumzia dhana ya Ujenzi mpya (Rebuilding) alisisitiza umuhimu wa kujifanyia tathimini kwa kuangalia mapungufu yaliyopo na kuyafanyia kazi na kusonga mbele katika kusukuma maendeleo.

Kama Taifa ni muhimu kuitumia dhana ya 4R katika kusukuma maendeleo. Kwa dhana hii inaungatia historia yetu uhalisia na kutupeleka  mbele (Historic, Realistic and Futuristic) na kwamba  inaunganisha historia ya nchi yetu kwa kulinganisha na hali halisi ya  sasa ili kusonga mbele zaidi katika mafanikio.


SERIKALI YABORESHA MAZINGIRA YA WAFANYABIASHARA WADOGO (MACHINGA)

"Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuboresha mazingira ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wadogo (Machinga, Mama lishe, Baba lish...